Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

KIHENZILE AWATAKA WADAU WA AUTOEXPO KUCHANGAMKIA FURSA ZA UWEKEZAJI SEKTA YA UCHUKUZI

Imewekwa: 20 Nov, 2026
KIHENZILE AWATAKA WADAU WA AUTOEXPO KUCHANGAMKIA FURSA ZA UWEKEZAJI SEKTA YA UCHUKUZI

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, amewataka wadau wa sekta ya magari, mitambo na vipuri kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazotokana na maboresho ya miundombinu ya uchukuzi yanayofanywa na Serikali nchini.

Mhe. Kihenzile ametoa wito huo leo, Novemba 18, 2026, jijini Dar es Salaam, alipomwakilisha Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, kufungua Maonyesho ya Autoexpo yanayofanyika Novemba 18–20, 2026, katika viwanja vya Diamond Jubilee.

Naibu Waziri Mhe. Kihenzile amesema maboresho ya reli, barabara, bandari na viwanja vya ndege yanafungua fursa nyingi za biashara na uwekezaji, huku akisisitiza kuwa Serikali iko tayari kushirikiana na sekta binafsi kwa kuzingatia umuhimu wake katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Maonyesho hayo yameshirikisha takribani kampuni 135 zinazoonesha bidhaa na huduma mbalimbali zinazohusiana na magari, mitambo, vipuri na teknolojia zake.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Maonyesho ya Autoexpo, Duncan Njage, amesema maonesho hayo ni jukwaa muhimu la kuwaunganisha wadau wa ndani na nje ya nchi, kuonesha teknolojia mpya na kukuza fursa za kibiashara katika sekta ya magari na mitambo.

Mkurugenzi wa Masoko ya Ndani na Nje wa TanTrade, Bi. Doroth Urio, aliyemwakilisha Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, amesisitiza umuhimu wa maonesho hayo katika kutangaza bidhaa, kupanua masoko na kuimarisha ushirikiano kati ya wafanyabiashara na wawekezaji.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Automobile Association of Tanzania (AAT), Bi. Najma Rashid, ameeleza umuhimu wa sekta ya magari katika kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya sekta ya uchukuzi, akihimiza wadau kutumia maonesho hayo kujenga ushirikiano na kutafuta fursa mpya.

Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi ili kukuza uwekezaji, biashara, uhamishaji wa teknolojia na ajira kwa Watanzania, huku wadau wakihimizwa kutumia maonesho hayo kujenga mahusiano ya kibiashara na kuchangamkia fursa zilizopo nchini.