Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

NAIBU KATIBU MKUU WA UCHUKUZI APONGEZA MAFANIKIO YA TPA.

Imewekwa: 20 Sep, 2026
NAIBU KATIBU MKUU WA UCHUKUZI APONGEZA MAFANIKIO YA TPA.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Bw. Abdallah Mitawi, ameipongeza TPA kwa mafanikio yaliyopatikana, huku akisisitiza kuongeza ufanisi, tija na ubora wa huduma

Akizungumza wakati wa ziara yake Makao Makuu ya TPA jijini Dar es Salaam tarehe 17 Septemba, 2026 amesema bandari ni mhimili wa uchumi wa Taifa, ikichangia takribani asilimia 40 ya mapato yanayokusanywa na TRA na kuitaka TPA kutumia vyema fursa ya kijiografia ya nchi, kuoanisha mipango yake na  Dira 2050, vipaumbele vya Serikali pamoja na kuimarisha maandalizi dhidi ya mabadiliko tabianchi ikiwemo athali za mvua za El nino ili kuhakikisha usalama na mwendelezo wa huduma za bandari za Tanzania kikanda

Amesema ongezeko la shughuli za bandari limeongeza mahitaji ya huduma na kuweka shinikizo kwenye miundombinu iliyopo hata hivyo Serikali inaendelea na ujenzi, upanuzi na uboreshaji wa miundombinu, sambamba na kushirikisha sekta binafsi

Awali, Naibu  Mkurugenzi  Mkuu  wa TPA Mha.Dkt. Baraka Mdima alitoa maelezo kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo na kuelezea hali ya utendaji na mikakati ya kuimarisha huduma za bandari

Akitoa wasilisho, Meneja wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa TPA Bw. Alfred Matuntela amesema TPA inasimamia bandari 135 na kuhudumia Tanzania pamoja na nchi nane za kikanda, zikiwemo DRC, Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi na Uganda na kuongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano, idadi ya meli imeongezeka kutoka 4,751 hadi 6,002, shehena kutoka tani mil.20.78 hadi tani mil. 39.90, makasha kutoka TEUs 823,404 hadi 1,381,598, huku mapato yakiongezeka kutoka Shilingi tril. 1.14 hadi 1.58