Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

KIHENZILE: UWANJA WA NDEGE TANGA KUFUNGUA FURSA ZA UWEKEZAJI

Imewekwa: 20 Sep, 2026
KIHENZILE: UWANJA WA NDEGE TANGA KUFUNGUA FURSA ZA UWEKEZAJI

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema kukamilika kwa mradi wa ujenzi na ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Tanga kutafungua fursa mpya za kiuchumi, kuongeza uwekezaji na kuboresha huduma za usafiri wa anga katika Mkoa wa Tanga na maeneo ya jirani.

Akikagua maendeleo ya mradi huo, Naibu Waziri Kihenzile ameeleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa na kusema Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga ili kuchochea maendeleo na kuwanufaisha wananchi.

Naibu Waziri Kihenzile ameongeza kua uwanja huo utakapokamilika utarahisisha usafiri wa abiria na mizigo, kuimarisha shughuli za biashara na utalii, pamoja na kuongeza mchango wa sekta ya usafiri katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga Mhandisi Msama Msama amesema mkandarasi anaendelea na kazi kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa na kwamba hakuna sababu ya kuongeza muda wa utekelezaji wa mradi huo. Alieleza kuwa usimamizi wa karibu unaendelea kufanyika ili kuhakikisha kazi zote zinakamilika kwa ubora na ndani ya muda uliokubaliwa.

Naye Msimamizi wa Uwanja wa Ndege wa Tabora Bi Hana Kibopile amesema maboresho ya miundombinu ya viwanja vya ndege nchini yamechangia kuongezeka kwa idadi ya abiria na mashirika ha ndege yanayotumia Kiwanja hicho kwa safari za ratiba na zisizo za ratiba.