Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

MABORESHO BANDARI YA DAR ES SALAAM YAONGEZA SHEHENA, MAPATO

Imewekwa: 20 Sep, 2026
MABORESHO BANDARI YA DAR ES SALAAM YAONGEZA SHEHENA, MAPATO

Maboresho yanayoendelea katika Bandari ya Dar es Salaam yameanza kuzaa matunda kwa kuongeza ufanisi wa huduma, kuvutia meli zaidi na kuchochea ongezeko la shehena pamoja na mapato ya bandari hiyo.

Akizungumza katika kikao cha maboresho ya Bandari (PIC) kilichofanyika katika ukumbi wa TPA jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, amesema uwepo wa vifaa vya kisasa na kuimarika kwa kasi ya kuhudumia meli kumeongeza idadi ya meli zinazoingia bandarini.

Prof. Kahyarara amesema ongezeko hilo linahitaji ushirikiano zaidi wa wadau ili kuhakikisha mizigo inayoshushwa bandarini inatolewa kwa wakati na kuongeza ufanisi wa mnyororo wa usafirishaji.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu, Rogatus Mativila, amesema Serikali kupitia TARURA inaendelea kuboresha barabara zinazounganisha bandari kavu na maeneo mengine ili kurahisisha usafirishaji wa shehena.

Naye Meneja Uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Frank Korasa, amesema kiwango cha shehena kinachopita bandarini kimeongezeka kwa kiasi kikubwa, huku DP World ikiendelea kuwekeza katika mitambo ya kisasa na kuboresha maeneo ya kuhifadhia mizigo ili kuongeza ufanisi wa huduma bandarini.