Naibu Waziri Kihenzile aipongeza TPA
Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile imeipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kuendelea kuboresha uendeshaji wa bandari nchini, hatua iliyoongeza ufanisi, uwajibikaji na ubora wa huduma, sambamba na kuimarisha mchango wa bandari katika kukuza uchumi wa taifa.
Akizungumza mkoani Pwani baada ya kutembelea Bandari ya Nyamisati, Naibu Waziri Kihenzile, amesema maboresho yanayotekelezwa na TPA yameifanya sekta ya bandari kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi kwa kuongeza kasi ya kuhudumia mizigo, kupunguza muda wa meli kukaa bandarini na kuboresha mazingira ya biashara.
Aidha, ameongeza kuwa hatua hizo zimeendelea kuongeza mapato ya Serikali na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama lango muhimu la biashara na usafirishaji wa mizigo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Naibu Waziri Kihenzile ameitaka TPA kuhakikisha miradi ya ujenzi wa bandari za Bagamoyo, Kisiju na Nyamisati inawanufaisha wananchi moja kwa moja kupitia utekelezaji wa miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR), ikiwemo huduma za kijamii na uboreshaji wa miundombinu katika maeneo yanayozunguka bandari.
Kuhusu usafiri wa uhakika katika bahari kuu, Naibu Waziri Kihenzile amesema Serikali kupitia Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) inaendelea na tafiti za kitaalamu ili kubaini mahitaji halisi, kama sehemu ya maandalizi ya kuchukua hatua za kuimarisha usafiri majini nchini.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus, amesema maboresho yanayotarajiwa kufanyika ni pamoja na uboreshaji wa jengo la abiria ili liweze kuhudumia abiria 300 kwa wakati mmoja, pamoja na ujenzi na uboreshaji wa miundombinu mingine ya bandari.
